Jumanne, 7 Mei 2013

MAALIM SEIF ALAANI KITENDO CHA KULIPULIWA BOMU ARUSHA


Chama cha Wananchi CUF kimelaani vikali kitendo cha kulipuliwa kwa kanisa mkoani Arusha na kusababisha vifo na majeruhi kwa watu wasiokuwa na hatia.

Akizungumza na wananchi katika maeneo tofauti Mkoani Singida, Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, amekitaja kitendo hicho kuwa ni cha kinyama na kisichotarajiwa kutoa nchini Tanzania.

Amesema Tanzania ina historia ya kuwa nchi ya amani, na kwamba vitendo kama hivyo vinaitia doa na kuiharibia sifa yake Kitaifa na Kimataifa.Kufuatia tukio hilo, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amewataka wananchi kuacha kushutumiana na kuiachia serikali kufanya uchunguzi wa kina, ili kuwabaini waliohusika na kuwachukulia hatua za kisheria.

Ameishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya juhudi za makusudi za kuwaunganisha Watanzania ambao wanaonekana kuanza kusahau misingi yao ya asili ya kuishi kwa pamoja bila ya ubaguzi.

“Udini na ukabila vinaonekana kupiga hodi Tanzania, naiomba serikali kufanya juhudi za kuwaunganisha wananchi ili kuepukana na kitisho hiki ambacho ni hatari kwa nchi yetu”, alisema Maalim Seif.

Wakati huo huo Maalim Seif amekutana na Viongozi wa Baraza la Waislamu Mkoani Singida, na kuwaasa kuishi kwa pamoja na kushirikiana kama Watanzania.

“Kila mtu ana imani yake, lakini tukumbuke kuwa sisi sote ni Watanzania na kila mmoja ana haki sawa na mwengine, kwa hivyo tuishi kwa kuvuliana kama yanavyoamrisha mafunzo ya dini zote, kwani hakuna dini inayoamrisha maovu”, alifahamisha Maalim Seif.

Viongozi hao walikutana na Makamu wa Kwanza wa Rais kwa lengo la kumuelezea juu ya mipango yao ya kuendeleza shule ya Kiislamu ya “Kinyeto Muslim Profession”, pamoja na zahanati wa wanawake mkoani humo.

Mapema akizungumza katika mikutano ya hadhara iliyofanyika Ikungi na Singida Mjini, Maalim Seif amesema wakati umefika kwa watanzania kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kuachana na kilimo cha kutegemea mvua.

Amesema miaka 50 ya uhuru ni muda mrefu wa kurekebisha mipango ya maendeleo, na kwamba tatizo kubwa la uchumi wa Tanzania ni kutokuwepo mipango imara la kuendeleza uchumi kwa maslahi ya Taifa na wananchi.

Amesema Tanzania imejaaliwa kuwa na ardhi kubwa yenye rutba ambayo sehemu kubwa bado haijatumika ipasavyo katika kuendeleza kilimo cha kisasa cha umwagiliaji ambacho kinaweza kuwakomboa watanzania kujikwamua na umaskini.

Amesema iwacho CUF kitapewa mamlaka ya kuongoza nchi kitasimamia mipango hiyo ya kiuchumi na kuhakikisha kuwa kila Mtanzania ananufaika na rasilimali za nchi.

Kwa upande wake Mbunge wa viti maalum (CUF) kutoka Mkoa wa Tabora bibi Madelina Sakaya, amedai kuwa bado serikali haijatenga fedha za kutosha kwa miradi ya maendeleo, na badala yake imekuwa ikitenga fedha nyingi kwa ajili ya viburudhishaji maofisini.

Nae Naibu Mkurugenzi wa haki za binadamu, habari na uenezi wa CUF Bw. Abdul Kambaya amewataka wananchi wa Singida kutafakari kwa kina juu ya tatizo la umaskini unaowakabili, licha ya kuwa na shughuli nyingi za maendeleo zikiwemo kilimo cha alizeti, mifugo na biashara.

Ametaja baadhi ya sababu za kuwepo umaskini kuwa ni pamoja na elimu duni inayotolewa mashuleni, pamoja na mfumo mbaya wa uongozi ambao unahitaji kufanyiwa mabadiliko.

Hassan Hamad, OMKR.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni